Ibada katika madhabahu ya Moyo
Yohana 4:23-24
Lakini saa inakuja, nayo sasa ipo, ambayo waabuduo halisi watamwabudu Baba katika roho na kweli. Kwa maana Baba awatafuta watu kama hao wamwabudu. Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli.
Mungu ametuumba tumwabudu yeye peke yake kupitia maisha yetu ya kila siku. Kwa ujumla, kuna tafsiri nyingi za ibada kulingana na mitazamo mbalimbali ya watu na theolojia au mafundisho tofauti tofauti. Ibada ni jambo lolote au kitu chochote unachokiwaza, au kukinena, au kukitenda katika maisha yako. Ni vema kujua kuwa kila unalolifanya kuna Mungu anapokea utukufu mahala na kuwa ibada yako kwake ikiwa unajua ama hujui.
Kama utendalo ni jema Mungu wa mema atapokea ibada na kama ni mabaya basi mungu wa mabaya atapokea ibada yako. Na Mungu anayepokea ibada huwa anakupatia au anakuzawadia vilivyomo katika hazina yake mfano shetani katika hazina yake atakuzawadia tabia zake pamoja na uharibifu (Wagalatia 5:16-21; Yohana 8:44) vivyo hivyo Mungu akipewa ibada atakuzawadia tabia zake, uzima tele, pamoja na baraka zake (Wagalatia 5:22; Yohana 1:4-8; Waefeso 1:3). Hizo tabia au mambo Mungu wako atakupatia baada ya kupokea ibada yako yataathiri maisha yako ya nje na kutoa tafsiri nzima ya maisha yako.
Hivyo, maisha yako yote ni matokeo ya ibada unayoifanya na ukitaka kubadili mtindo au muundo wowote katika maisha badili kwanza ibada yako katika hilo eneo. Vivyo hivyo ukitaka kuboresha muundo au mtindo wowote katika maisha yako boresha kwanza ibada yako kwenye hilo eneo. Mithali 23:7 inasema aonavyo mtu nafsini mwake ndivyo alivyo. Hivyo ukitaka ubadili au uboreshe ulivyo lazima kwanza ubadili uonavyo nafsini mwako. Hiyo nafsi inayoongelewa ndio injini ya maisha yako na ndiyo mahala ibada inafanyika na wakati mwingine inaitwa moyo.
Yesu anaongea na mwanamke kisimani kuwa ibada halisi inapaswa kufanyika katika roho pasipo ya kufungwa na mazingira kama anavyonena katika Yohana 4:21 “Yesu akamwambia, Mama, unisadiki, saa inakuja ambayo hamtamwabudu Baba katika mlima huu, wala kule Yerusalemu.” Ukiunganisha na mistari inayofuata ya 23 na 24 utaona kuwa ibada anayoitaka Mungu kwa wakati huu ni ile inayofanyika rohoni kusikoonekana kwa macho wala kushikika kwa mikono.
Yerusalemu na mlima wa yakobo ilikuwa ni madhabahu zilizofanywa kwa mikono ya watu na kupitisha ibada. Lakini ibada ya katika roho yenyewe hutegemea madhabahu isiyoonekana inayoitwa Moyo, na ndio madhabahu bora ambayo kuhani wake ni wewe mwenyewe. Ukiitumia vema madhabahu ya moyo kiibada inakua na ushawishi mkubwa katika tafsiri ya maisha yako. Na ukikaa vema kwenye nafasi yako kama kuhani kwa madhabahu ya moyo na ukamfanyia Mungu ibada hakuna anayeweza kuzuia ibada yako.
Ipe thamani ipasayo ibada inayofanyika katika madhabahu ya moyo wako ili ufaidike kimaisha. Madhabahu ya moyo ikikaa sawa ibada yako na maisha yako yatakuwa sawa ila madhabahu ya moyo wako ikiharibika na ibada pia na maisha yako yataharibika (Mathayo 5:8). Ukisoma Mithali 4:23 imeandikwa “Linda moyo wako kuliko yote uyalindayo; Maana ndiko zitokako chemchemi za uzima.” ikiwa na maana ya kulinda Moyo kama madhabahu ya kiibada inayozalisha vitu katika maisha yako.
Kwa ujumla ibada imebeba tafsiri nzima ya maisha yako hivyo ithamini na kuilinda. Wewe kuwapo mahala fulani kifursa iwe kazini, katika familia, biashara, ndoa, kilimo au cheo kunategemea na ibada unayompatia Mungu aliyekuweka hapo. Ibada yako ikiyumba na nafasi yako lazima iyumbe tu hivyo ibada yako ndio usalama na mafanikio yako mahala ulipo. Shetani akitaka kukuangusha mahala ulipo au kukuondoa katika nafasi ulipo lazima aanze kwanza kugusa ibada yako kwa Mungu kwenye hilo eneo. Ibada yako katika nafasi uliyopo ina thamani kubwa sana hivyo ilinde.
Mifano ya vita ya shetani dhidi ya ibada yako kwa Mungu:
1. Vita ya Daniel katika nafasi ya uongozi (Daniel 6:1-28
Walipotafuta kumwondoa Danieli kwenye nafasi yake (Daniel 6:3) walitumia kila mbinu zikashindikana (Daniel 6:4-6) ndipo wakakubaliana kumbana katika muhimili wake ambao ni ibada yake kwa Mungu wake, soma ule mstari wa 7 “Mawaziri , watawala wamefanya shauri pamoja ili kuweka amri ya kifalme; na kupiga marufuku, ya kwamba mtu yeyote atakayeomba dua kwa Mungu awaye yote, au kwa mtu awaye yote, katika muda wa siku thelathini, ila kwako, Ee mfalme atatupwa katika tundu la simba.” Unaweza kuona dhahiri kuwa waligundua kuwa asili ya nguvu za Danieli ni ibada hivyo ilipaswa kushughulikiwa. Lakini Danieli hakukubali ibada yake yake na Mungu ife hivyo aliipambania na Mungu akajitwalia utukufu (Daniel 6:25-28). Swali la kujiuliza ni kwanini ibada ndiyo iwekewe sheria katika mkakati wa kumwondoa katika uongozi. Sasa inaweza kuangaliza kazini kwako, kwenye ndoa yako, biashara yako, je kuna sheria gani au kitu gani kinainuka juu ya ibada yako! Usikubalii kwa maana ibada yako ndio usalama wako!
2. Vita Hamani dhidi ya Mordekai kiibada (Esta 3:1 – 8:17)
Ukisoma kitabu cha Esta kiinaonesha vita ya Hamani dhidi ya wayahudi na jinsi Mungu alivyowatetea na kuuangamizia Hamani kwenye kitanzi alichokiandaa kwaajili ya kumtundika Mordekai. Lakini ukiangalia asili ya vita hii ni Mordekai kukaa kusujudu mbele ya Hamani. Ukisoma mistari kadhaa ya mlango wa tatu “Nao watumishi wote wa mfalme, walioketi langoni pa mfalme, wakainama na kumsujudia Hamani, maana ndivyo mfalme alivyoamuru wamfanyie. Lakini Mordekai hakumwinamia, wala kumsujudia. Hata Hamani alipoona ya kwamba Mordekai hamwinamii wala kumsujudia, alighadhibika sana. Akaona haitoshi kumtia mikono Mordekai peke yake; maana wamemjulisha kabila lake Mordekai; kwa hiyo Hamani alitaka kuwaangamiza Wayahudi wote waliokuwa wakikaa katika ufalme wote mzima wa Ahasuero, yaani, watu wake Mordekai.”
Hii ilikuwa ni test ya kutaka kuharibu ibada ya Mordekai kwa Mungu lakini haikuwezekana kumwangusha. Mungu anajihirisha na kumpigania Mordekai na wayaudi wote kinyume cha Hamani. Swali, Je ni kitu gani umekiabudu au kukisujuidia katika maisha yako? Utajiri, cheo, biashara ukaviinamia na kuvipatia ibada badala ya Mungu. Kumbe Mungu anasema usiwe na Miungu mingine ila Mimi. Yaani hata Yesu mwana wa Mungu alijaribiwa kwenye eneo la ibada ya kusujudia na kashinda hilo jaribu (Luka 4:6-8). Nawewe yakupasa ushinde jaribu la kusujudia au kuabudu vitu and nafasi fulani katika maisha yako
3. Vita dhidi ya Shadrack, Meshaki na abedinego kwenye kuabudu sanamu (Daniel 3:1-30)
Mungu aliwatetea hawa watu kwasabubu walikataa kuabudu sanamu ya Mfalme Nebukadreza. Mstari wa 18 “Bali kama si hivyo, ujue, Ee mfalme, ya kuwa sisi hatukubali kuitumikia miungu yako, wala kuisujudia hiyo sanamu ya dhahabu uliyoisimamisha.” Ukionesha wazi hawa watumishi wa Mungu walivyokuwa tayari kukabiliana na tanuru kuliko kupoteza ibada yao kwa Mungu. Ukisoma hadi mwisho wa mlango huu utaona Mungu alishuka mwenyewe kuwatetea na kujitwalia utukufu (Daniel 3:28-30). Je nini kimekutisha kimaisha na ukakubali kusaliti uhusuiano wakona Mungu na kumpatia ibilisi ibada yako? Kumbuka ibada ni kitu chochote unachokiwaza au kukinena au kukitenda.
Vita za ndani zinazopambana kuharibu ibada yako na Mungu katika madhabahu ya Moyo:
Hii ni vita hatari zaidi katika maisha yako ya Imani maana hutafuna ibada yako taratibu. Usipokuwa makini ni kuwa unapotea kimfumo bila kujua. Na ndio vita hatari zaidi dhidi ya ibada inayofanyika katika madhabahu ya moyo
1. Divided attention (Mathayo 15:8)
Shetani akitaka kuondoa thamani ya ibada yako na Mungu huwa anatumia njia ya kukuondolea umakini wako kwa ibada kwa kutumia vitu mbali mbali muda wa ibada. Moja ya kitu kikubwa katika maisha ya ibada katika madhabahu ni wewe kua na umakini na ibada muda wote na ndipo shetani anabana hapo. Mara nyingi unakuta muda wa ibada shetani anakuondoa kimawazo na kukupeleka nyumbani, unawaza madeni, unawaza maumivu ya kutendwa, yaani muda wa ibada madhabahu ya moyo unaijaza na makorokoro mengi kiasi kwamba inashindwa kufanya kazi yake.
Lakini pia unakuta muda wa ibada mtu yuko na simu anachati, anasoma meseji au anapokea simu yaani Mungu anasubiria wewe umalize kujibu meseji ndipo muendeleee na ibada. Mfano: Wewe fikiria ukiwa kama mzazi uko na mazungumzo na mtoto wako alafu yeye yuko busy anachati kwa simu yake utajisisikiaje? Ndivyo Mungu anajisikia ukitumia simu wakati wa ibada. Kwa ujumla muda wa ibada ni wa Mungu tuliza akili kwa Mungu 100%. Kitabu cha Mathayo 15:8 neno la Mungu linasema “Watu hawa huniheshimu kwa midomo; Ila mioyo yao iko mbali nami.” Ikiwa na maana Mungu anahitaji madhabahu ya Moyo wako imfanyie ibada kwa maana maneno matupu hayana nguvu kama moyo haupo. Divided attention ni vita kubwa Mno na inaathiri ibada za wengi.
2. Kutokuthamini ibada (Mwanzo 4:2-13)
Kutoipa ibada thamani inayostahili katika moyo wako, yaani kuona ibada ni kitu cha kawaida na wakati sio. Ibada ni maisha yako hivyo lazima ipewe thamani kubwa katika maisha yako na uifanye kwa moyo wakupenda. Unaweza kuona mfano wa watu wawili walioandaa ibada sawa katika biblia (Mwanzo 4) Kaini na Abeli, unaona kila mtu alipeleka sadaka kwa Mungu ila majibu yakawa tofauti tofauti. Ibada (sadaka) ya Kaini ilikataliwa kwasababu hakuithamini toka madhabahu ya moyo hivyo alitoa vilivyodhaifu wakati Abeli yeye alitoka kwa moyo wa kupenda vilivyo vinono sadaka kwa Mungu nayo ikapokelewa.
Angalia Mwanzo 4:4-5 Habili naye akaleta wazao wa kwanza wa wanyama wake na sehemu zilizonona za wanyama. BWANA akamtakabali Habili na sadaka yake; bali Kaini hakumtakabali, wala sadaka yake. Kaini akaghadhibika sana, uso wake ukakunjamana. Ni maeneo Mengi umekunjamana uso wako kwasababu ya mafanikio ya wenzako maofanya kazi sawa ila wao wanafanikiwa wakati wewe hufanikiwi na umesingizia uchawi, uganga, hakuna uchawi fanya ibada yenye thamani kupitia kazi yako Mungu ataipokea na kukubariki tu.
3. Kujihesabia haki (Luka 18:10-14)
Ukisoma katika kitabu kile cha Luka (18:10-14) Yesu anatoa mfano wa watu wawili waliokwenda hekaluni kwaajili ya ibada mmoja mfarisayo (mtu wa dini) na mtoza ushuru ambaye ni mwenye dhambi kwa tafsiri ya wakati ule. Mstari wa 11 unaonesha haya maombi yalikuwa moyoni yaani katika madhabahu ya moyo na mfarisayo alitumia ibada hiyo kujisifia na kujilinganisha na watu wengine. Hili liliharibu ibada yake kwa Mungu kabisaa ukilinganisha na Mtoza ushuru aliyeshuka na kuomba msamaha kwa Mungu.
Yesu anahitimisha kwa kusema Luka 18:14 “Nawaambia, huyu alishuka kwenda nyumbani kwake amehesabiwa haki kuliko yule; kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa.”. Swali je ni mara ngapi umejihesabia haki mbele za Mungu wakati wa ibada? Mara ngapi umeona wengine ni wadhambi hivyo hawana thamani mbele za Mungu kiibada? Usikubali madhabahu ya moyo wako ikainua kujihesabia haki, huyo ni shetani anapiga vita ibada yako. Ona neno la Mungu katika kitabu cha 1 Peter 5:5b “…; kwa sababu Mungu huwapinga wenye kiburi, lakini huwapa wanyenyekevu neema.”
4. Kukosa Utii (Mwanzo 3:4)
Kukosa utii ni lango kubwa sana shetani hutumia kuharibu ibada yako na Mungu. Yaani kwa ufupi haya yeye kilichomtoa Mbinguni ni kutokutii utawala Mungu na kutaka aabudiwe kama Mungu (Isaya 14:12-15). Alitumia namna hiyo hiyo kumwagusha mwanadamu kiibada katika bustani ya edeni, mwanadamu akaamua kutotii maelekezo ya Mungu na kula tunda la mti wa Katikati ili awe kama Mungu (Mwanzo 3:1-22). Hata sasa shetani bado anapambana sana na madhabahu ya moyo wako ili usiweze kutii maelekezo ya Mungu katika maisha yako ili kuharibu ibada yako alafu uanguke mahala ulipo kifursa au kimaisha. Mungu anathamini sana ibada yako ikiwa inafuata maelekezo yake na sio matakwa ya kibinadamu.
Samweli anamwambia Sauli katika kitabu kile cha (1 Samwel 15:22) “Naye Samweli akasema, Je! BWANA huzipenda sadaka za kuteketezwa na dhabihu Sawasawa na kuitii sauti ya BWANA? Angalia, kutii ni bora kuliko dhabihu, Na kusikiza ushauri kuliko mafuta ya bebeeru”. Shetani akipiga kutii kwako amepiga ibada yako na amepiga maisha yako kwa ujumla katika eneo hilo. Swali: Je mara ngapi Mungu amesema nawe kwa habari ya maisha yako nawe hukutii? Mambo yakiharibika usisingizie wachawi, rekebisha utii wako kwanza. Ukimpa Mungu utii katika maelekezo yake yeye anakuinua na kukupa jina lake kama ilivyokuwa kwa Yesu kitabu kile cha wafilipi 2: 5-11. Lakini pia atakukuza na kukubariki sanaa kaatika eneo hilo kama alivyofanya kwa Ibrahimu alipokubali kutii kumtoa mwanae Isaka awe sadaka (Mwanzo 22)
Ibada yako katika moyo ina thamani kubwa ndio maana shetani anaiwinda sana kwasababu imebeba tafsiri ya maisha yako. Usikubali ibada yako ikaharibika ama kupotea maana itakuwa ndio kupotea kwako kimaisha. Mungu akupe neema ya kuithamini na kuipambania ibada yako kwa Mungu katika madhabahu ya moyo wako kama kuhani ili ikutete na kukunufaisha kimaisha.
Ibada katika madhabahu ya Moyo Read More »
